Agizo la RTO Arusha kwa Mabasi ya abiria laanza kutekelezwa, Atoa onyo kwa Wamiliki wa Malori


Na Gasto Kwirini wa Jeshi la Polisi Arusha

Ikiwa ni siku ya tatu tangu kuanza kwa operesheni ya ukaguzi wa magari Mkoani Arusha, leo tarehe 11.07.2019 muda wa asubuhi imebainika baadhi ya Wamiliki, Madereva na Makondakta wameanza kuitikia wito wa kutozidisha abiria katika mabasi yao na kufuata sheria bila kushurutishwa.

Operesheni hiyo inayoongozwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi (SP)Joseph Bukombe imeanza kuonyesha matokeo chanya baada ya ukaguzi kufanyika katika Mabasi yanayofanya safari zake kati ya Arusha na Kiteto, ambapo hayakuzidisha abiria kama ilivyozoeleka kwa mabasi mengi yanayopita njia hiyo.

Akitolea mfano Basi la Kampuni ya Mtei Express, Mkuu huyo wa Usalama barabarani ameipongeza kampuni hiyo, dereva pamoja na Kondakta  kwa kuitikia wito wake alioutoa kwa wamiliki, madereva na Makondakta kwa kuhakikisha wanafuata Sheria za usalama barabarani, ambapo mabasi mengi yalikua yanajaza Abiria kuliko uwezo wa gari.

"Kwanza  nimpongeze mmiliki wa Mabasi ya Mtei, nadhani Elimu ya Utii wa Sheria bila shuruti ameanza kuifanyia kazi, leo tumekuja mpaka Custom na tumekuta basi lake likiwa levo siti, namuomba aendelee kufanya ivo ivo hatagombana na Jeshi la Polisi lakini akizidisha abiria tunageuka hadi kituoni tunaanza moja  na Abiria wote waliozidi atawatafutia usafiri mwingine". Alisema RTO wakati akizungumza na Abiria wa Basi hilo..

Sambamba na hilo amefanya ukaguzi wa malori yanayobeba mchanga katika maeneo mbalimbali hasa katika barabara ya Arusha - Simanjiro/Kiteto  na kubaini ubovu mkubwa katika malori hayo hasa uchakavu wa matairi.

Amesema zoezi la ukaguzi wa Malori hayo amelianza rasmi na atafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha malori yote mabovu hayapiti barabarani. Pia wamiliki wa magari hayo kuyafanyia matengenezo hasa kuyafunga tairi mpya kwani mengi tairi zimeisha.

"Zoezi la kukagua malori ya mchanga linaanza upya, na leo tumewafuata uku wanakochukua mchanga  lengo ni kuhakikisha kwamba malori hayo yanarudi katika hali nzuri kama zoezi tulilolifanya mwaka ambapo tuliagiza wayatengeneze na walifanya ivyo, sasa naona wamejisahau". Alisisitiza RTO.

Aidha amesisitiza kwamba endapo watayafanyia matengenezo magari yao, madereva wao watafanya kazi kwa uhuru bila usumbufu wakiwa  barabarani.

Naye Wakala wa Mabasi ya Mtei Express Bwana amepongeza Operesheni, amesisitiza iwe endelevu kwani itasaidia kuwakumbusha Wamiliki kukagua magari yao kila mara pamoja na kuwadhibiti madereva, na Makondakta wanaovunja sheria. 

Theophil Fredrick Makala, Dereva na Mkazi wa Kwamrombo, amelishukuru Jeshi la polisi kwa ukaguzi wanaondelea kuufanya kwani inasaidia magari yao kuwa salama kwani inapelekea wamiliki wa magari kuyajali hasa kuyatengeneza kila mara na pia ukaguzi huo unawafanya wao kuwa na nidhamu kwa kufuata sheria za usalama barabarani.

Jumla ya Malori matano yamekamatwa na  kufikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha kwa ajili ya kufanyiwa  Ukaguzi zaidi ili yaweze kuadhibiwa kwa mujibu wa Sheria.

1. Picha No. 1. Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi (SP) Joseph Bukombe akishuka katika basi baada ya kulifanyia ukaguzi ambao unaendelea Mkoani Arusha

2. Picha No. 2. Vijana wakisukuma noja kati ya lori bovu ambalo limekamatwa na Jeshi la Polisi katika Operesheni inayoendelea ya ukaguzi wa magari Mkoani Arusha.

3. Picha No. 3. Moja kati ya tairi ya Lori ambayo inaonekana ikiwa katika hali ya uchakavu ambapo limekamatwa katika Operesheni ya ukaguzi wa Magari inayoendelea Mkoani Arusha

4. Picha No. 4. Baadhi ya malori yaliyokamatwa kwa ubovu katika Operesheni ya Ukaguzi wa Magari inayoendelea kufanyika mkoani Arusha.

0 Comments